Kuwa na afya bora ni jambo muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Kama una matatizo ya afya hutaweza kutimiza majukumu yako ya kila siku, hivyo maisha yako hayatakuwa katika hali nzuri.
Sote tunajua huwezi kufanya chochote pale
unapokuwa mgonjwa na masuala ya afya yanahusisha zaidi mazingira
yanayotuzunguka. Ni ukweli kwamba mazingira yetu yakiwa machafu basi
afya zetu zitakuwa katika hatari kubwa, kwani uchafu ndiyo mahali
mwafaka kwa wadudu wasababishao magonjwa kuzaliana na kustawi.
Ni jambo la kusikitisha kuwa Watanzania wengi
hatujali mazingira yanayotuzunguka. Elimu ya kutosha imetolewa kwa njia
za mikutano ya kijamii, vyombo vya habari na njia nyinginezo, lakini
haieleweki kinachotokea kama ni kutojali au ni kweli kutoelewa. Hebu
tuzitafakari tabia hizi.
Unaweza kukuta mtu amevaa vizuri, anapendeza
lakini ukienda kuangalia mahali anapotoka yaani nyumbani kwake,
utashangaa. Kumejaa uchafu usiofanana na kupendeza kwa mtu huyo. Mtu
mtanashati ndiye utakuta anakula ndizi barabarani na maganda akayatupa
hapo barabarani bila kujali kwamba atavutia inzi waletao maradhi.
Mtu huyu mtanashati ndiye anayetupa uchafu
barabarani akiwa ndani ya daladala bila kujali nani atauokota, kama
kweli utaokotwa. Usafi ni tabia, kama ni tabia ina maana mtu atakuwa
msafi katika nyendo zake zote, iweje sasa mtu awe msafi katika nguo
alizovaa halafu akatupa taka ovyo, kwa nini asijimwagie takataka
mwenewe.
Bila shaka mtu huyu ni mnafiki, hata mavazi hayo
masafi ni kwa ajili ya kujionyesha tu. Kama kungekuwa hakuna mtu wa
kumwangalia, bila shaka hata nguo zake zingekuwa chafu.
Utakuta watu na akili zao wanauza chakula pembeni
mwa mifereji ya maji machafu. Wakati mwingine utakuta mtu anafanya usafi
sehemu anayofanyia biashara na kuzisukuma takataka pembeni au upande wa
pili wa barabara. Watu wa namna hii wanafikiria inzi nao wanaijua
mipaka yao.
Bila kujali, utakuta mtu anaukaribisha ugonjwa wa
kipindupindu kwa kufanya vitendo vya kinyama kabisa; kwani ni vitendo
vya uuaji. Utakuta katika kipindi cha mvua mtu anatumia mwanya wa
kunyesha mvua kwa kuzibua choo chake na kuelekeza uchafu wote
barabarani.
Watoto wanatembea pekupeku, wadudu wanazaliana na
magonjwa nje nje. Cha kushangaza uchafu huo unaelekezwa kwenye barabara
ambayo hata yeye na familia yake wanapita. akati mwingine ni watoto wake
ndiyo wanaoetembea pekupeku. Wakipata maradhi, ataishia kulalamika
kwamba wanawe wamerogwa. Hakumbuki vitendo vichafu alivyofanya. Ukiuliza
ni kwa nini watu wanaishi na uchafu watakwambia kwamba Serikali
imeshindwa kutoa takataka hizo; sababu ya kawaida kwa Watanzania
wasiotaka kutimiza wajibu wao.
Kama nilivyosema hapo mwanzo usafi ni tabia, hivyo
hauendeani na usomi, utajiri au sifa nyingine. Wapo watu wenye uwezo
ambao nao wana tabia zinazochangia kufanya mazingira yawe machafu. Hawa
unakuta wanajenga ukuta kuzuia njia ya maji, hivyo kusababisha kero na
madhara ya kiafya kwa watu wananowazunguka.
Kwa kutumia uwezo wa kifedha wanaziba kabisa njia
za maji machafu, hivyo kulazimisha maji hayo kuishia kwenye nyumba za
watu wanaowazunguka na wenyewe wanaona ni sawa kabisa.
Wengine ni wasomi wazuri lakini usomi wao
unashindwa kuwafafanulia kwamba kipindupindu kitakapofumuka, hata wao
wapo hatarini kwani hawaruki kwa helikopta kwenda majumbani kwao.
Yaani utakuta maji yenye kemikali hatari yanatiririka kuelekea
kwenye makazi ya watu na kusababisha harufu kali na hatari ya magonjwa
kama vile saratani na mengineyo. Utaona maji machafu yenye rangi za
ajabu na harufu kali yakitiririka kwenye makazi ya watu.
Watu hawa wanatumia fedha nyingi kuhonga wenye
mamlaka ili wasiwachukulie hatua, badala ya kutumia fedha hizo
kutengeneza miundombinu itakayosaidia kusafirisha majitaka kwa usalama
zaidi. Ni tabia za uchafu ndiyo zinazowasumbua na kuwafanya watenda
vitendo vya kuchafua mazingira
Tunaweza kufikiri ni gharama kuweka mazingira yetu
safi, lakini ukweli ni kwamba ni gharama kubwa zaidi kutibu madhara
yanayosababishwa na mazingira machafu. Ukipata magonjwa kwanza shughuli
zako zinasimama, pili unatumia muda na fedha nyingi kujitibia, hii yote
ni hasara kubwa kwako.
Lakini hasara kubwa kuliko zote ni kwamba, unaweza
kupoteza maisha yako na hakuna gharama inayoweza kuifidia maisha. Kwani
ungetumia gharama gani kushughulikia maji machafu ukilinganisha na
kuharisha wiki nzima?
Mwisho utaona kile kidimbwi kinasababisha mlolongo
wa hasara juu ya hasara. Na hapo bado tutaililia Serikali kweli ni
sahihi hii?
Ni wakati sasa Watanzania tubadilike na kujali
mazingira yanayotuzunguka kwani mazingira bora maana yake afya bora na
hakuna maendeleo, bila afya bora. Huu ni wajibu wetu sote kama kweli
tunataka kupiga hatua.
0 comments:
Post a Comment